Kaseha Wilson Mengi
Biography
KITAALUMA: KASEHA, Wilson Mengi alisoma Shahada ya Umahiri ya Ufuatiliaji na tathimini chuo kikuu cha Mzumbe Morogoro Tanzania. Ni Mwanasayansi ya Maabara za afya Tiba aliyesajiliwa na baraza la Usajili wa wanataaluma wa Sayansi ya Maabara Afya Tiba Tanzania. Alisoma shahada yake ya kwanza ya Sayansi ya Maabara za Afya Tiba Chuo kikuu cha Ki-Kristo cha Kilimanjaro (KCMUCo). Alisoma Stashahada ya Teknolojia ya Maabara za Afya Tiba nchini Kenya Chuo cha Kisumu (Kisumu Polytechnic).
Amefanya Kazi ya Uhadhiri, Ukuu wa Idara ya Sayansi ya Maabara katika Kitivo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Kimataifa Cha Kampala nchini Tanzania (Kampala International University in Tanzania - KIUT) kwa zaidi ya miaka sita (6).
Amekuwa Msimamizi Mkuu wa mitihani (Chief Examination Supervisor) ya NACTVET kwa vyuo vya kati mpaka hivi leo. Ni Mjumbe wa timu za ukaguzi vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi chini ya NACTVET.
Amewahi kuwa Mratibu wa huduma/shughuli za kimaabara wa Wilaya ya Hai-Kilimanjaro kwa zaidi ya miaka minane (8)
Amekuwa Meneja wa Maabara ya Wilaya ya Hai kwa muda wa miaka mitatu (3)
MAISHA & HUDUMA KANISANI: KASEHA, Wilson Mengi, ambaye kwa sasa ni Katibu wa AICT Dayosisi ya Geita, alimpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa maisha yake tangu mwaka wa 1991 akiwa na umri wa miaka 10, na alibatizwa mwaka 1993 na Mchungaji Yusuph Ngunda wa Pastoreti ya Irunda.
Alizaliwa na Mama aitwaye Joyce Daud Clement Kaseha wa familia ya Mzee Daud Clement Kaseha aliyekuwa Mzee wa Kanisa na Mhasibu wa kanisa la Irunda kwa muda mrefu. Kaseha, Wilson Mengi alikuwa ni mtoto pekee kwa zaidi ya miaka kumi kabla ya mama yake kupata watoto wengine wawili (Tambilija & Daud). Alipata neema ya kuzaliwa na kukua akiwa katika nyumba ya babu yake Mkristo wa AICT na hivyo kupata nafasi ya kujifunza na kujua mengi yahusuyo Imani ya Kristo katika maisha ndani ya Kanisa la AICT.
Amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Kanisa la Mungu; amewahi kuwa Katibu wa Kanisa na Pastoreti ya Ukonga AICT kwa Zaidi ya miaka miwili. Amewahi kuwa Mzee wa kanisa, -Nyampulukano, Mhudumu na Mzee wa kanisa la AICT-Ukonga na KKKT Hai – Kilimanjaro. Amewahi kuwa Mwenyekiti Msaidizi Idara ya Vijana ngazi ya Pastoreti -Ukonga, pia amekuwa Katibu wa Vijana ngazi ya Jimbo Sengerema-Mlimani. Kaseha, ni mwanakwaya wa muda mrefu.